Hebrews 9:9-28

9 aHuu ulikuwa mfano kwa ajili ya wakati wa sasa, kuonyesha kwamba sadaka na dhabihu zilizokuwa zikitolewa hazikuweza kusafisha dhamiri ya mtu anayeabudu. 10 bLakini hizi zilishughulika tu na vyakula na vinywaji, pamoja na taratibu mbalimbali za kunawa kwa nje, kanuni kwa ajili ya mwili zilizowekwa hadi wakati utimie wa matengenezo mapya.

Damu Ya Kristo

11 cKristo alipokuja akiwa Kuhani Mkuu wa mambo mema ambayo tayari yameshawasili, alipitia kwenye hema iliyo kuu zaidi na bora zaidi, ambayo haikutengenezwa kwa mikono ya binadamu, hii ni kusema, ambayo si sehemu ya uumbaji huu. 12 dHakuingia kwa njia ya damu ya mbuzi na ya ndama; lakini aliingia Patakatifu pa Patakatifu mara moja tu kwa damu yake mwenyewe, akiisha kupata ukombozi wa milele. 13 eDamu ya mbuzi na ya mafahali, na majivu ya mitamba walivyonyunyiziwa wale waliokuwa najisi kwa taratibu za kiibada viliwatakasa, hata kuwaondolea uchafu wa nje. 14 fBasi ni zaidi aje damu ya Kristo, ambaye kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na waa, itatusafisha dhamiri zetu kutokana na matendo yaletayo mauti, ili tupate kumtumikia Mungu aliye hai!

15 gKwa sababu hii Kristo ni mpatanishi wa agano jipya, ili kwamba wale walioitwa waweze kupokea ile ahadi ya urithi wa milele: kwa vile yeye alikufa awe ukombozi wao kutoka kwa dhambi walizozitenda chini ya agano la kwanza.

16Kwa habari ya wosia,
Wosia hapa kwa neno la Kiyunani ni agano.
ni muhimu kuthibitisha kifo cha yule aliyeutoa,
17 ikwa sababu wosia huwa na nguvu tu wakati mtu ameshakufa; kamwe hauwezi kutumika wakati yule aliyeuandika bado yuko hai. 18 jHii ndiyo sababu hata lile agano la kwanza halikuweza kutekelezwa pasipo damu. 19 kMose alipotangaza kila amri kwa watu wote, alichukua damu ya ndama na ya mbuzi, pamoja na maji, sufu nyekundu na matawi ya mti wa hisopo, akanyunyizia kile kitabu na watu wote. 20 lAlisema, “Hii ndiyo damu ya agano, ambalo Mungu amewaamuru kulitii.” 21 mVivyo hivyo alinyunyizia damu hiyo kwenye ile hema pamoja na kila kifaa kilichotumika ndani yake kwa taratibu za ibada. 22 nKwa kweli sheria hudai kwamba, karibu kila kitu kitakaswe kwa damu, wala pasipo kumwaga damu, hakuna msamaha wa dhambi.

23 oKwa hiyo, ilikuwa muhimu kwa nakala za vitu vile vya mbinguni vitakaswe kwa dhabihu hizi, lakini vitu halisi vya mbinguni vilihitaji dhabihu bora kuliko hizi. 24 pKwa maana Kristo hakuingia kwenye patakatifu palipofanywa kwa mikono ya mwanadamu, ambao ni mfano wa kile kilicho halisi. Yeye aliingia mbinguni penyewe, ili sasa aonekane mbele za Mungu kwa ajili yetu. 25 qWala hakuingia mbinguni ili apate kujitoa mwenyewe mara kwa mara, kama vile kuhani mkuu aingiavyo Patakatifu pa Patakatifu kila mwaka kwa damu ambayo si yake mwenyewe. 26 rIngekuwa hivyo, ingempasa Kristo kuteswa mara nyingi tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Lakini sasa ametokea mara moja tu katika mwisho wa nyakati aiondoe dhambi kwa kujitoa mwenyewe kuwa dhabihu. 27 sKama vile mwanadamu alivyowekewa kufa mara moja tu na baada ya kufa akabili hukumu, 28 tvivyo hivyo Kristo alitolewa mara moja tu kuwa dhabihu ili azichukue dhambi za watu wengi. Naye atakuja mara ya pili, sio kuchukua dhambi, bali kuwaletea wokovu wale wanaomngoja kwa shauku.

Copyright information for SwhNEN